| Chapter 12 |
1 |
Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake. -
|
2 |
Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, "Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato." -
|
3 |
Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? -
|
4 |
Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao. -
|
5 |
Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia? -
|
6 |
Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu*fd* kuliko Hekalu. -
|
7 |
Kama tu mngejua maana ya maneno haya: `Nataka huruma wala si dhabihu`, hamngewahukumu watu wasio na hatia. -
|
8 |
Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato." -
|
9 |
Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao. -
|
10 |
Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, "Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?" Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki. -
|
11 |
Lakini Yesu akawaambia, "Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato? -
|
12 |
Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato." -
|
13 |
Kisha akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine. -
|
14 |
Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu. -
|
15 |
Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote, -
|
16 |
akawaamuru wasiwaambie watu habari zake, -
|
17 |
ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: -
|
18 |
"Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote. -
|
19 |
Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani. -
|
20 |
Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale. -
|
21 |
Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini." -
|
22 |
Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona. -
|
23 |
Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, "Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?" -
|
24 |
Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, "Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo." -
|
25 |
Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka. -
|
26 |
Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje? -
|
27 |
Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi. -
|
28 |
Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. -
|
29 |
"Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake. -
|
30 |
"Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya. -
|
31 |
Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. -
|
32 |
Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. -
|
33 |
"Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake. -
|
34 |
Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni. -
|
35 |
Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya. -
|
36 |
"Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema. -
|
37 |
Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia." -
|
38 |
Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako." -
|
39 |
Naye akawajibu, "Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona. -
|
40 |
Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha. -
|
41 |
Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona! -
|
42 |
Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu*fe* kuliko Solomoni. -
|
43 |
"Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate. -
|
44 |
Hapo hujisemea: `Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.` Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa, -
|
45 |
huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu." -
|
46 |
Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye. -
|
47 |
Basi, mtu mmoja akamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe." -
|
48 |
Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, "Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?" -
|
49 |
Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, "Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu! -
|
50 |
Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu." -
|