| Chapter 24 |
1 |
Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu. -
|
2 |
Yesu akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa." -
|
3 |
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?" -
|
4 |
Yesu akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. -
|
5 |
Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye Kristo,` nao watawapotosha watu wengi. -
|
6 |
Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado. -
|
7 |
Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi. -
|
8 |
Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto. -
|
9 |
"Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu. -
|
10 |
Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana. -
|
11 |
Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi. -
|
12 |
Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia. -
|
13 |
Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka. -
|
14 |
Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote. -
|
15 |
"Basi, mtakapoona `Chukizo Haribifu` lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake), -
|
16 |
hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani. -
|
17 |
Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake. -
|
18 |
Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. -
|
19 |
Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! -
|
20 |
Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato! -
|
21 |
Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena. -
|
22 |
Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa. -
|
23 |
"Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: `Kristo yuko hapa` au `Yuko pale,` msimsadiki. -
|
24 |
Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. -
|
25 |
Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati. -
|
26 |
Basi, wakiwaambieni, `Tazameni, yuko jangwani,` msiende huko; au, `Tazameni, amejificha ndani,` msisadiki; -
|
27 |
maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. -
|
28 |
Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. -
|
29 |
"Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. -
|
30 |
Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi. -
|
31 |
Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu. -
|
32 |
"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. -
|
33 |
Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.*fk* -
|
34 |
Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. -
|
35 |
Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. -
|
36 |
"Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye. -
|
37 |
Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. -
|
38 |
Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina. -
|
39 |
Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja. -
|
40 |
Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. -
|
41 |
Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. -
|
42 |
Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu. -
|
43 |
Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. -
|
44 |
Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia." -
|
45 |
Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake? -
|
46 |
Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo. -
|
47 |
Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote. -
|
48 |
Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: `Bwana wangu anakawia kurudi,` -
|
49 |
kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi, -
|
50 |
bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua. -
|
51 |
Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno. -
|