| Chapter 13 |
1 |
Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!" -
|
2 |
Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa." -
|
3 |
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, -
|
4 |
"Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?" -
|
5 |
Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. -
|
6 |
Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi. -
|
7 |
Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. -
|
8 |
Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. -
|
9 |
"Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao. -
|
10 |
Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. -
|
11 |
Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. -
|
12 |
Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. -
|
13 |
Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. -
|
14 |
"Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani. -
|
15 |
Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. -
|
16 |
Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. -
|
17 |
Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! -
|
18 |
Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. -
|
19 |
Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. -
|
20 |
Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. -
|
21 |
"Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki. -
|
22 |
Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana. -
|
23 |
Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. -
|
24 |
"Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. -
|
25 |
Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. -
|
26 |
Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. -
|
27 |
Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. -
|
28 |
"Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. -
|
29 |
Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. -
|
30 |
Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. -
|
31 |
Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. -
|
32 |
"Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. -
|
33 |
Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. -
|
34 |
Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho. -
|
35 |
Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. -
|
36 |
Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. -
|
37 |
Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!" -
|