| Chapter 2 |
1 |
Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe. -
|
2 |
Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. -
|
3 |
Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake. -
|
4 |
Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi. -
|
5 |
Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito. -
|
6 |
Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, -
|
7 |
akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. -
|
8 |
Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. -
|
9 |
Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. -
|
10 |
Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote. -
|
11 |
Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. -
|
12 |
Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini." -
|
13 |
Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: -
|
14 |
"Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!" -
|
15 |
Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha." -
|
16 |
Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. -
|
17 |
Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake. -
|
18 |
Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji. -
|
19 |
Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake. -
|
20 |
Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa. -
|
21 |
Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. -
|
22 |
Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana. -
|
23 |
Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana." -
|
24 |
Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana. -
|
25 |
Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. -
|
26 |
Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana. -
|
27 |
Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria, -
|
28 |
Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema: -
|
29 |
"Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani. -
|
30 |
Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako, -
|
31 |
ambao umeutayarisha mbele ya watu wote: -
|
32 |
Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli." -
|
33 |
Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto. -
|
34 |
Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu; -
|
35 |
na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako." -
|
36 |
Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa. -
|
37 |
Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana. -
|
38 |
Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu. -
|
39 |
Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya. -
|
40 |
Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye. -
|
41 |
Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. -
|
42 |
Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. -
|
43 |
Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. -
|
44 |
Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. -
|
45 |
Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. -
|
46 |
Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. -
|
47 |
Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. -
|
48 |
Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni." -
|
49 |
Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?" -
|
50 |
Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. -
|
51 |
Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. -
|
52 |
Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. -
|