| Chapter 3 |
1 |
Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo. -
|
2 |
Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye." -
|
3 |
Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu." -
|
4 |
Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!" -
|
5 |
Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. -
|
6 |
Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. -
|
7 |
Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. -
|
8 |
Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho." -
|
9 |
Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?" -
|
10 |
Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya? -
|
11 |
Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu. -
|
12 |
Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni? -
|
13 |
Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni. -
|
14 |
"Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo, -
|
15 |
ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele. -
|
16 |
Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. -
|
17 |
Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu. -
|
18 |
"Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu. -
|
19 |
Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. -
|
20 |
Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. -
|
21 |
Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu." -
|
22 |
Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu. -
|
23 |
Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza. -
|
24 |
Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.) -
|
25 |
Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha. -
|
26 |
Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng`ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea." -
|
27 |
Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu. -
|
28 |
Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: `Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!` -
|
29 |
Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa. -
|
30 |
Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue. -
|
31 |
"Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote. -
|
32 |
Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake. -
|
33 |
Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli. -
|
34 |
Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo. -
|
35 |
Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote. -
|
36 |
Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake." -
|