| Chapter 10 |
1 |
Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang`anyi. -
|
2 |
Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. -
|
3 |
Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje. -
|
4 |
Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake. -
|
5 |
Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake." -
|
6 |
Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. -
|
7 |
Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. -
|
8 |
Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang`anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza. -
|
9 |
Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho. -
|
10 |
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili. -
|
11 |
"Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. -
|
12 |
Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya. -
|
13 |
Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. -
|
14 |
Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi, -
|
15 |
kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao. -
|
16 |
Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. -
|
17 |
"Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. -
|
18 |
Hakuna mtu anayeninyang`anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye." -
|
19 |
Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. -
|
20 |
Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?" -
|
21 |
Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?" -
|
22 |
Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. -
|
23 |
Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. -
|
24 |
Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi." -
|
25 |
Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. -
|
26 |
Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu. -
|
27 |
Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. -
|
28 |
Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. -
|
29 |
Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. -
|
30 |
Mimi na Baba, tu mmoja." -
|
31 |
Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. -
|
32 |
Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?" -
|
33 |
Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu." -
|
34 |
Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: `Mimi nimesema, ninyi ni miungu?` -
|
35 |
Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. -
|
36 |
Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: `Unakufuru`, eti kwa sababu nilisema: `Mimi ni Mwana wa Mungu?` -
|
37 |
Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini. -
|
38 |
Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake." -
|
39 |
Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. -
|
40 |
Yesu akaenda tena ng`ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. -
|
41 |
Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa." -
|
42 |
Watu wengi mahali hapo wakamwamini. -
|