| Chapter 11 |
1 |
Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. -
|
2 |
Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: -
|
3 |
"Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! -
|
4 |
Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: -
|
5 |
"Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu. -
|
6 |
Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. -
|
7 |
Kisha nikasikia sauti ikiniambia: `Petro amka, chinja, ule.` -
|
8 |
Lakini mimi nikasema: `La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.` -
|
9 |
Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: `Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.` -
|
10 |
Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. -
|
11 |
Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa. -
|
12 |
Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. -
|
13 |
Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: `Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. -
|
14 |
Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.` -
|
15 |
Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. -
|
16 |
Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: `Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.` -
|
17 |
Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?" -
|
18 |
Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!" -
|
19 |
Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. -
|
20 |
Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu. -
|
21 |
Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. -
|
22 |
Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. -
|
23 |
Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. -
|
24 |
Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. -
|
25 |
Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo -
|
26 |
Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. ic -
|
27 |
Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. -
|
28 |
Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala). -
|
29 |
Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. -
|
30 |
Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo. -
|