| Chapter 1 |
1 |
Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. -
|
2 |
Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. -
|
3 |
Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. -
|
4 |
Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, -
|
5 |
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. -
|
6 |
Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu katika Mwanae mpenzi! -
|
7 |
Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake -
|
8 |
aliotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote -
|
9 |
Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. -
|
10 |
Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. -
|
11 |
Kila kitu hufanywa kufuatana na mpango na uamuzi wa Mungu; naye Mungu ametuteua sisi tuwe watu wake kwa mapenzi yake katika kuungana na Kristo, kufuatana na azimio alilofanya tangu mwanzo. -
|
12 |
Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! -
|
13 |
Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonyesha kuwa ninyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. -
|
14 |
Huyu Roho ni dhamana ya kurithi yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake! -
|
15 |
Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu na mapendo yenu kwa watu wa Mungu, -
|
16 |
sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu -
|
17 |
ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. -
|
18 |
Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, -
|
19 |
mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na nguvu ile kuu mno -
|
20 |
aliyomfufua nayo Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni. -
|
21 |
Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. -
|
22 |
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. -
|
23 |
Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali. -
|