| Chapter 2 |
1 |
Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. -
|
2 |
Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. -
|
3 |
Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu," -
|
4 |
je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya? -
|
5 |
Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda. -
|
6 |
Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani? -
|
7 |
Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa? -
|
8 |
Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa. -
|
9 |
Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia. -
|
10 |
Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote. -
|
11 |
Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria. -
|
12 |
Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. -
|
13 |
Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu. -
|
14 |
Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? -
|
15 |
Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. -
|
16 |
Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? -
|
17 |
Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa. -
|
18 |
Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. -
|
19 |
Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. -
|
20 |
Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa? -
|
21 |
Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu. -
|
22 |
Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. -
|
23 |
Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu." -
|
24 |
Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake. -
|
25 |
Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine. -
|
26 |
Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa. -
|