| Chapter 9 |
1 |
Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu. -
|
2 |
Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu. -
|
3 |
Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng`e. -
|
4 |
Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso. -
|
5 |
Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng`e. -
|
6 |
Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia. -
|
7 |
Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. -
|
8 |
Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba. -
|
9 |
Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani. -
|
10 |
Walikuwa na mikia na miiba kama ng`e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano. -
|
11 |
Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi. -
|
12 |
Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata. -
|
13 |
Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu. -
|
14 |
Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa `Eufrate!"` -
|
15 |
Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu. -
|
16 |
Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili. -
|
17 |
Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao. -
|
18 |
Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao; -
|
19 |
maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu. -
|
20 |
Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea. -
|
21 |
Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi. -
|