| Chapter 17 |
1 |
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, "Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi. -
|
2 |
Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake." -
|
3 |
Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. -
|
4 |
Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake. -
|
5 |
Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo "Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani." -
|
6 |
Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno. -
|
7 |
Lakini malaika akaniambia, "Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi. -
|
8 |
Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena! -
|
9 |
"Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba. -
|
10 |
Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi. -
|
11 |
Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa. -
|
12 |
"Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. -
|
13 |
Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote. -
|
14 |
Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme." -
|
15 |
Malaika akaniambia pia, "Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha. -
|
16 |
Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. -
|
17 |
Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia. -
|
18 |
"Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala wafalme wa dunia." -
|