| Chapter 22 |
1 |
Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. -
|
2 |
Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. -
|
3 |
Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. -
|
4 |
Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. -
|
5 |
Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele. -
|
6 |
Kisha malaika akaniambia, "Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde. -
|
7 |
"Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki." -
|
8 |
Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. -
|
9 |
Lakini yeye akaniambia, "Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!" -
|
10 |
Tena akaniambia, "Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. -
|
11 |
Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu." -
|
12 |
"Sikiliza!" Asema Yesu, "Naja upesi, pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. -
|
13 |
Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho." -
|
14 |
Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya kula tunda la mti wa uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. -
|
15 |
Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji. -
|
16 |
"Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!" -
|
17 |
Roho na Bibiarusi waseme, "Njoo!" Kila mtu asikiaye hili, na aseme,"Njoo!" Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yoyote. -
|
18 |
Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. -
|
19 |
Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang`anya sehemu yake katika ule mti wa uzima, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. -
|
20 |
Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: "Naam! Naja upesi." Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu! -
|
21 |
Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen. -
|